Quantcast
Channel: SUFIANIMAFOTO
Viewing all articles
Browse latest Browse all 13053

*HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR, MHE. BALOZI SEIF A. IDDI KATIKA UWEKAJI WA JIWE LA MSINGI JENGO JIPYA LA ABIRIA (TERMINAL 11) NA NJIA YA MAEGESHO YA NDEGE

$
0
0
Mheshimiwa Rashid Seif Suleiman, Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano,
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Mheshimiwa Katibu Mkuu, Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini/Magharibi, Unguja,
Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania,
Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi - Zanzibar.
Waheshimiwa Viongozi mbali mbali wa Vyama vya Siasa na Serikali,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
 Asaalam Aleykum,
 Ndugu Wananchi,
Awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kuwa wazima wa afya na kutuwezesha  kukusanyika hapa kwa lengo la kuadhimisha sherehe  za miaka  hamsini (50) ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar katika uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa jengo jipya la abiria (Terminal II) na pamoja  na njia  na maegesho ya ndege  (Taxway and Apron).
Pia napenda kuushukuru Uongozi wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kwa heshima kubwa walionipa kwa kunialika kuwa Mgeni Rasmi katika shughuli hii muhimu ambayo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari, 1964.
Ndugu Wananchi, KUSOMA ZAIDI BOFYA READ MORE

Ujenzi wa  jengo jipya la  abiria (Terminal II) pamoja  na njia na maegesho ya ndege (taxway na apron) ni miongoni mwa  juhudi zinazochukuliwa na  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuimarisha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume ili kiweze kufikia hadhi ya juu ya Kimataifa katika  kutoa huduma kwa abiria na ndege zinazoingia na kutoka  kwa lengo la kuimarisha uchumi wa nchi yetu kwa manufaa ya wananchi wote wa Zanzibar.  Ujenzi wa jengo jipya  la  abiria  pamoja  na ujenzi wa njia na maegesho ya ndege ni miongoni mwa hatua ya  utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2010- 2015 ambazo tulikuwa  tukizinadi kwenu  wakati wa kipindi cha kuomba ridhaa kutoka kwenu  ya kuiongoza nchi hii, miongoni mwa ahadi ni kwamba  tutaimarisha huduma za kiwanja cha ndege cha Abeid Amani Karume ili kiweze kufikia hadhi ya Kimataifa na leo hii tunathibitisha utekelezaji  wa ahadi  zetu kwa uwekaji  wa jiwe la msingi la ujenzi wa jengo jipya la abiria (Terminal II) ambalo litakuwa na uwezo wa kuchukuwa abiria 1,600,000 kwa mwaka na huduma zote zinazositahiki kwa abiria pamoja  na njia  na maegesho ya ndege  ambayo  itakuwa na  uwezo  wa kukaa  ndege  aina  ya  CODE E. 3 na CODE C. 5 – yaani ndege za aina ya Boeing 737 na 777.
Ndugu Wananchi,
Nimeelezwa kwamba mradi wa ujenzi wa Terminal (II) umeanza rasmi tarehe 10 Januari, 2011 na unategemewa kukamilika mwezi wa nne, 2015.  Aidha, ujenzi  wa jengo jipya la abiria linalojengwa na Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group Co. Ltd. kutoka nchini China na chini ya uangalizi wa  Kampuni ya ADPI kutoka Ufaransa, unategemewa kutumia jumla ya Dola 82.6 Million ambazo  ni mkopo kutoka kwa Washirika wa Maendeleo (Exim Bank) kutoka China. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inachangia jumla ya T.Shs:  2,000,000,000.
Kwa upande  wa ujenzi wa njia na maegesho ya ndege, ujenzi wake unatekelezwa na  Kampuni ya  M/S SOGEA – SATOM na ulianza rasmi tarehe  20 Agosti, 2012 na unategemewa kukamilika tarehe 15 Mei, 2014 chini ya usimamizi wa Kampuni ya JBG Gauff  Ingineure GmbH & Co. KG in Association  with  M/s  NIMETA  Consulting (T) kutoka Tanzania na unategemewa kutumia jumla ya T.Shs: 75.8 Bilioni hadi kukamilika kwake ambazo ni mkopo  kutoka  Benki ya Dunia. Aidha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inachangia T.Shs. 1.36 Bilioni katika  mradi huo.
 Miradi hii itakapokamilika itapelekea kuimarisha uchumi wa nchi yetu kwani  kutakuwa na kiwango kikubwa cha ndege  za Kimataifa zitakazoingia  hapa  nchini  ikiwemo za mizigo  na abiria.  Aidha, sekta ya utalii ambayo ndio sekta kuu kwa uchumi wa Zanzibar itaimarika na kupelekea kukua kwa uchumi  wa Taifa letu.  Lengo la Serikali katika sekta ya utalii ni kupokea zaidi ya watalii 250,000 ifikapo mwaka 2015.  Kwa hivyo, mradi huu utasaidia sana kufikia lengo hilo.
Vile vile, wafanyabiashara wadogo wadogo nao, biashara zao zitaimarika na kupata kipato ambacho kitawapunguzia ukali wa maisha.  Ni matumaini yangu kuwa jengo hili litakapokamilika  litatoa  nafasi nyingi za ajira ambapo wajasiriamali wataitumia nafasi  hii  kuimarisha shughuli zao za kibiashara ili kupunguza umasikini wa kipato na hatimae kuweza kujipatia mahitaji yao ya msingi.  
 Ndugu Wananchi,
Serikali ya awamu ya saba  kwa muda mfupi imeweza kutekeleza kwa kiwango kikubwa Ilani ya Uchaguzi, licha ya hali ngumu ya uchumi inayoikabili nchi yetu.   Naomba nichukuwe fursa hii kueleza kwa muhtasari, juhudi zinazochukuliwa na   Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha huduma za viwanja vya ndege, Zanzibar. Serikali ilichukuwa hatua ya kuanzisha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kwa lengo la kuboresha huduma za viwanja vya ndege ili ziendane na hadhi ya Kimataifa.   Aidha, Serikali tayari imeshajipanga kuimarisha miundombinu ya Kiwanja cha ndege cha Pemba kwa kuweka taa katika kiwanja hicho ili kiweze kutoa huduma wakati wa usiku, kwa sasa hivi kiwanja hicho kinatoa huduma wakati wa mchana tu kiasi ambacho ni tatizo kubwa kwani ikitokea dharura ya kwenda au kuondoka Pemba wakati wa usiku au imetokea dharura ya aina yoyote ile, huwa ni tatizo kwa sababu ya ukosefu wa taa za kuongozea ndege wakati wa kuruka na kutua katika kiwanja cha ndege cha Pemba.  Serikali inajitahidi kwa kila njia ili kuhakikisha kuwa kiwanja hicho nacho kinakidhi haja.
 Ndugu Wananchi,
Juhudi hizi zinazochukuliwa na Serikali zinachangiwa kwa kiasi kikubwa na umoja na mshikamano uliopo hapa Zanzibar katika kutekeleza majukumu yetu. Ni imani yangu kuwa juhudi hizi tutazidumisha na kuziendeleza kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya nchi yetu. Sote tunafahamu kuimarika kwa viwanja vya ndege ndio chachu ya maendeleo kwa sekta nyengine za kiuchumi kama vile utalii na biashara.  
 Ndugu Wananchi,
Kwa kipindi cha miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar, huduma za viwanja vya ndege zimeimarika hapa Zanzibar na kuongezeka kwa Makampuni  mbali mbali ya Kitaifa na Kimataifa yanayotoa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo nje na ndani ya Tanzania. 
 Hizi zote ni juhudi kubwa  zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo na Muundo wa Umoja wa Kitaifa katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar pamoja na kuimarisha uchumi wa Visiwa vya  Zanzibar.
 Ndugu Wananchi,
Mafanikio yote haya yanatokana na uongozi makini, uadilifu mkubwa, ujasiri wa hali ya juu, ubunifu, mashirikiano na usimamizi mzuri tulionao katika kutekeleza majukumu yetu.  Aidha, amani iliyopo Zanzibar pamoja na mshikamano wa Kitaifa uliojengeka miongoni mwa Wazanzibari, umesaidia sana kupatikana kwa mafanikio hayo. Kwani bila ya amani na utulivu hakuna maendeleo.  Nawaomba wananchi wote nchini wawe wadau wa kuendeleza amani na utulivu wa nchi yetu.
 Ndugu Wananchi,
Sasa napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kwa kusimamia na kutekeleza majukumu iliyopewa kwa vitendo na kwa ufanisi mkubwa.  
Aidha, naipongeza kwa dhati Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Zanzibar kwa kuimarisha huduma zinazositahiki katika viwanja vya ndege, nawaomba waendelee na moyo huo huo wa kusimamia majukumu yao vizuri kwa lengo la kuwahudumia wananchi Watanzania na nchi nyengine kwa ujumla.
 Napenda pia kuupongeza uongozi mpya wa uwanja wa ndege kwa kuboresha mazingira ya uwanja na kuutaka uongozi huo kuzidisha juhudi na ubunifu ili uwanja wetu uwe miongoni mwa viwanja vya ndege vyenye usalama wa hali ya juu wa abiria na usafi wa hali ya juu. Ninayo mifano hai ya viwanja vyengine nje ya nchi ambapo utawakuta wafanyakazi wa usafi wanafanya kazi muda wote wa kazi.  Kila saa ufyagio mkononi, wafanyakazi wetu lazima waige mfano huu.
Kwa kipekee kabisa, napenda kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Ndugu Said Ndumbogani pamoja na Meneja wake kwa kuugeuza uwanja huu na kuwa katika hali iliyo sasa, ambao umejaa haiba na kupendeza.  Aidha, nautaka Uongozi wa Mamlaka kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa uwanja wa ndege kwa lengo la kuwa na uwezo wa kuwahudumia abiria kwa muda mfupi – shorter check-in times kama inavyowezekana bila ya kuathiri usalama wao na wa abiria.
Pia napenda kuwapongeza kwa dhati TCRA kwa kusimamia usalama wakati wote katika eneo la viwanja vya ndege, Zanzibar.  Nawaomba wazidishe mashirikiano yao kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Zanzibar kwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.  Vile vile, nawaomba wajenzi wa jengo jipya la abiria pamoja na njia na maegesho ya kutulia ndege kuhakikisha kuwa mradi huu unakamilika kwa wakati uliopangwa.  Pia, nawaomba wasimamizi wa ujenzi  wa miradi yote miwili kufanya kazi kwa umakini mkubwa na kuhakikisha tunapata jengo jipya la abiria (Terminal II) la kisasa, njia na maegesho ya ndege (Taxway and Apron) zenye kiwango kinachokubalika.
 Napenda pia kutoa shukrani zangu za dhati  kwa Mshirika  wetu wa Maendeleo  hasa  Exim Benki ya China na Benki ya Dunia kwa kutuunga mkono katika kutekeleza mipango ya maendeleo ya wananchi wa Zanzibar. Nawaomba waendelee kushirikiana nasi katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kutupatia, misaada na mikopo yenye masharti nafuu. 
 Nawaomba wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa mjenzi wakati watakapo hitajika kufanya hivyo kwa lengo la kufanikisha kazi hii kwa wakati.  Vile vile, nawaomba Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kuweka mipaka ya Viwanja vya Ndege Unguja na Pemba kwa lengo la kuepusha uvamizi wa maeneo ya viwanja vya ndege.  Hivyo, ningependa kutoa wito kwa wananchi kuheshimu mipaka ya uwanja wa ndege na kujiepusha na kujenga karibu na uwanja huo, jambo ambalo linaweza kuleta usumbufu wakati Serikali inapotaka kufanya upanuzi wa uwanja huo.
 Ndugu Wananchi,
Napenda niwapongeze wale wote walioandaa shughuli hii muhimu na kunialika mimi kujumuika nanyi nikiwa Mgeni Rasmi, shughuli ambayo imetayarishwa vizuri na hivyo kufana sana.  Aidha, nawapongeza na kuwashukuru wananchi wote ambao wamekuja kwa wingi katika sherehe hii.  Naamini kuwa kwa juhudi hizi, wananchi wana kila sababu ya kutuamini na kujenga imani juu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya saba kwa kuwapatia maendeleo ya kweli wananchi wa Zanzibar.
 Ndugu Wananchi, mwisho ningependa kuwashukuru, msoma quraan, ambaye amesoma aya zenye mnasaba na shughuli yetu hii. Pia nawapongeza wasoma utenzi kwa umalenga wao na kutupa burudani nzuri.
 Ndugu Wananchi,
Kwa kumalizia napenda nichukue fursa hii tena kuwapongeza wananchi wote kwa kuhudhuria kwa wingi katika shughuli hii.  Naomba Mwenyezi Mungu atuzidishie upendo na utulivu pamoja na kuipenda nchi yetu.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.                       

Viewing all articles
Browse latest Browse all 13053

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>