Na Mwandishi Wetu, Tanga
MABINGWA wa Soka Ligi Kuu ya Bara, Yanga Sc, jana wameangukia pua na kurudi hatua moja nyuma katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Mgambo JKT katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga jana.
Hadi mapumziko tayari Mgambo JKT walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililofungwa na Fully Maganga katika dakika ya kwanza tu ya mchezo akimalizia pasi ya Bashiru Chanacha.
Lilikuwa ni shuti la ghafla lililopigwa na mchezaji huyo mara tu baada ya kupata pasi, na kumshitukiza kipa Juma Kaseja, aliyekuwa hajajiandaa kuucheza mpira huo na kumpita kiulaini.
Katika dakika ya 30, Mgambo ilipata pigo baada ya mchezaji wake, Mohamed Neto kutolewa nje kwa kadi mbili za njano, ya kwanza akikataa kukaguliwa na Mwamuzi Alex Mahagi na ya pili kuzozana na mwamuzi huyo akipinga kusachiwa kama amebeba hirizi.
Dakika ya 32 kipa wa Mgambo, Saleh Tendega aliumia na nafasi yake kuchukuliwa na Tony Kavishe.
Kipindi cha pili Yanga SC walirudi kwa nguvu na kufanikiwa kusawazisha bao kwa penalti iliyopigwa na Nahodha wake, Naddir Haroub 'Canavaro' katika dakika ya 52, baada ya beki wa Mgambo kuunawa mpira katika eneo la hatari.
Baada ya bao hilo Mgambo walicharuka na dakika ya 63, walifanikiwa kupata bao la ushindi.
Bao hilo lilifungwa kwa penalti na Malimi Busungu baada ya yeye mwenyewe kuangushwa kwenye eneo la hatari na beki wa Yanga SC, Kevin Yondan.
Matokeo hayo yanaifanya Azam iendelee kubaki kileleni ikiwa na jumla ya Pointi 53 baada ya mechi 23, wakati Yanga SC ikibaki na pointi 46 baada ya mechi 22.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Juma Kaseja, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Frank Domayo, Simon Msuva/Hamisi Kiiza dk77, Hassan Dilunga, Didier Kavumbangu, Mrisho Ngassa/Hussein Javu dk61 na Emmanuel Okwi.
Mgambo JKT; Saleh Tendega/Tony Kavishe dk32, Salim Mlima, Salim Gilla, Bashiru Chanacha, Bakari Mtama, Novatus Lukunga, Mohammed Samatta, Peter Mwalyanzi/Awadh Yassin dk88, Mohamed Neto, Fully Maganga na Malimi Busungu.
Kwingineko, Katika mchezo wa Simba dhidi ya Azam, Simba walilala mabao 2-1 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, na katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Mbeya City, iliiadhibu Tanzania Prisons, kwa bao 1-0.
Kwingineko, Katika mchezo wa Simba dhidi ya Azam, Simba walilala mabao 2-1 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, na katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Mbeya City, iliiadhibu Tanzania Prisons, kwa bao 1-0.