
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta amesema mjadala kuhusu taarifa za sura ya kwanza na ya sita ya Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unatarajia kuanza wiki ijayo katika Bunge hilo.
Sitta alisema hay leo katika ukumbi wa Bunge hilo mjini Dodoma baada baadhi ya wajumbe kumwomba kuchangia mjadala wakati ripoti hizo zikiendelea kuwasilishwa.
Alisema mdajala wa kuchangia sura hizo utaanza mara baada ya Kamati 12 za Bunge Maalum la Katiba kuwasilisha taarifa zao za sura ya kwanza na ya sita kuhusu Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge hilo.
Aliongeza kuwa kwa kujibu wa Kanuni ya namba 33(6) ambayo inasema baada ya Hoja za taarifa za Kamati namba moja hadi namba Kumi na Mbili kutolewa katika Bunge Maalum na Mwenyekiti kuelekeza hoja hizo zijadiliwe , mjadala kuhusu taarifa hizo utaanza.
Mwenyekiti huyo aliwataka baadhi ya wajumbe hao kusubiri mpaka uwasilishaji wa taarifa hizo utakapokamilika ndio watapata nafasi ya kuchangia kwa muda mrefu na kuwezesha wajumbe wengi kupata nafasi hiyo.