Na Magreth Kinabo, Dodoma
Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Profesa Mark Mwandosya amependekeza kwamba suala la rushwa litambuliwe Katiba Mpya, inayopendekezwa ili kuweza kuongeza nguvu ya kupambana nalo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mwandosya, ambaye pia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalum) wakati akichangia mjadala wa kujadili sura zilizobakia za Rasimu ya Katiba Mpya kwenye kikao cha thelasini na saba cha Bunge hilo linaloendelea mjini Dodoma, ambacho kinaendelea na sura ya Pili, Tatu, Nne na Tano za Rasimu hiyo.
Mhe. Mwandosya alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akichangia sura ya Tatu kuhusu Maadili ,Miiko ya Uongozi na Utumishi wa Umma.
“ Lazima suala la rushwa litambuliwe katika Katiba hii.Serikali zote mbili zitatunga sheria ili tuweze sasa kupigana na adui rushwa. Ni suala la kwetu sote halina muungano, lazima litambuliwe vinginevyo hii vita tutashindwa,” alisisitiza Mhe. Mwandosya.
Akizungumzia kuhusu suala la rushwa mjumbe mwingine wa Bunge hilo, Mhe. Dkt. Mary Mwanjwela akichangia sura hiyo alisema rushwa ni adui wa haki dunia nzima na Tanzania inaelewa pia ni sehemu ya utawala bora.
“Hili ni jambo linalorudisha maendeleo nyuma.Mimi ninawaomba wajumbe wenzangu tuliingize katika Katiba tusipoliingiza tutakuwa hatueleweki,” alisema Dkt. Mwanjwela.
Aidha Mhe. Mwandosya alisisitiza katika sura ya pili kupata bidhaa na huduma bora zenye viwango ni jambo muhimu.
Aliongeza kuwa kiuchumi Serikali itachukua hatua zinazofaa… ili kuwezesha ushindani wenye hali ya tija.
“ Regulation liwe kwenye Katiba itakuwa ni mapinduzi… si suala la Serikali bali la vyombo maalum,” alisema.
Profesa Mwandosya akichangia kuhusu sura ya Nne inayohusu Haki za Binadamu alisema mazingira safi ni suala mtambuka ni vema kuwa katika Katiba, kila Mtanzania kupata maji safi na salama, hivyo Katiba inaweza kusema kwani ni jambo la kitaifa ambalo litafanikiwa kwa kuwa ni wajibu wa Serikali , lakini si kwa kuipeleka mahakamani.
Alizungumzia pia kuhusu nyumba na makazi bora ni haki ya binadamu inaendana na mazingira safi na salama, hivyo likiwekwa katika Katiba ni lazima kila Mtanzania ataishi katika mazingira safi na salama.