Na Magreth Kinabo,Dodoma
Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, ambaye pia ni mwanasiasa mkongwe nchini , Mzee Kingunge Ngomabale Mwiru amesema Katiba bora ni ile itakayozingatia historia mafanikio ya miaka 50 iliyopita na Muungano imara.
Kauli hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Mzee Kingunge wakati akichangia katika mjadala wa Bunge hilo juu ya uwasilishaji wa taarifa za Kamati Namba Moja hadi Kamati Namba Kumi na Mbili za Bunge hilo kuhusu uhakiki wa Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa.
Aidha Mzee Kingunge amesema wameondosha mapendekezo ambayo yanataka kusambaratisha muungano ili uweze kuwa imara.
Mzee Kingunge aliyataja mambo matatu ambayo yatazingatia Katiba bora kuwa ni ni ile itakayoimarisha historia ya mafanikio ya miaka 50 iliyopita, inayopunguza na kuondoa kero mbalimbali za msingi.
Aliongeza kuwa tatu ni “Lazima Katiba Mpya iingize mambo ambayo yataimarisha nafasi za wananchi mfano wakulima , wafugaji, wavuvi, wasanii na wachimbaji wadogo… Tanzania haitakuwa kama ilivyokuwa huko nyuma baada ya mkutano huu.
“ Kwa sababu makundi yote yote yamekutana hapa kuzungumzia maslahi yao na hatma yao,” alisema Mzee Kingunge.
Mzee Kingunge alisema mawazo yaliyotolewa na ni ushindi mkubwa, kazi iliyobaki ni kupitisha.
“Kazi hii si ndogo ni kubwa…kwani kuna zogo
, lakini tumevulia napenda iandikwe kwa wino wa dhahabu kama ilivyo hapa ndani,” alisisitiza.
Mwanasiasa huyo alifafanua kuwa Katiba ni maridhiano, hivyo anajua wakubwa wataendelea kuzungumza, hivyo katika hilo ni vizuri wakawa waangalifu.
“ Tuifanye kazi hii kwa unyenyekevu, wananchi wanangoja Katiba bora,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalum la Katiba,Mhe. Andrew Chenge alisema wakati akihitimisha mjadala huo, si rahisi kuweka mambo yote kama yalivyotolewa na baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo, bali itachukua yale ya msingi mengine yatazingatiwa katika Sheria za Nchi.
Aliwaasa Watanzania kuisoma Rasimu ya Katiba Mpya iliyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na ile Rasimu ya Katiba Mpya iliyopendekezwa na Bunge hilo.
Ninyi ndio mtakaoamua ukweli uko wapi? Tumeboresha hakuna kazi ya kuweka koma tumekuja kuandika Katiba ya Watanzania.
Mhe. Chenge alisema Kamati yake ni wajumbe ambao ni hazina kwa Tanzania.
Kwa upande wake, mjumbe wa Bunge hilo, Mhe. Profesa Mark Mwandosya alisema kazi iliyofanywa na Bunge hilo imefanywa kwa uadilifu, hivyo wamezingatia Rasimu ya Katiba Mpya ya Tume na wameboresha kwa kuzingatia maslahi ya wananchi.