Quantcast
Channel: SUFIANIMAFOTO
Viewing all articles
Browse latest Browse all 13053

*TGDC NA KAMPUNI YA TOSHIBA WATILIANA SAINI MKATABA WA MAELEWANO (MOU) WA UTAFUTAJI WA NISHATI YA JOTOARDHI

$
0
0

Na Benedict Liwenga-MAELEZO.

Shirika la Uendelezaji wa Nishati ya Jotoardhi Tanzania (TGDC) pamoja na Kampuni ya TOSHIBA ya nchini Japan zimetiliana saini Mkataba wa Maelewano wa kufanya tafiti kwa pamoja zinahusu maeneo yenye viashiria ya upatikanaji wa nishati ya jotoardhi.

Utiaji saini wa mkataba huo umefanyika Desemba 4, 2015 Jijini Dar es Salaam katika Ofisi za TGDC ambapo hatua hiyo itaiwezesha TGDC kuweza kupata msaada wa kitaalam ambao utaliwezesha shirika hilo kuweza kuchimba ardhini kwa lengo la kupata mvuke utakaoweza kuzalisha umeme.

Akiongea ofisini kwake, Meneja Mkuu wa TGDC, Mhandisi Boniface Njombe amesema kuwa kupitia Serikali ya Japan hususani Shirika la Maendeleo Japan (JICA), Kampuni ya TOSHIBA watasaidia kuomba ufadhili wa Serikali yao ili kuweza kuendeleza ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme pamoja na matumizi mengine yanayoendana na nishati hiyo.

“Katika utafiti wa nishati ya jotoardhi tunahitaji watu wenye elimu na uzoefu na ujuzi wa kutosha, miongoni mwa makubaliano ndani ya mkataba huu tuliosaini leo ni wafanyakazi wetu kadhaa kuwapeleka nchini Japan kwenye vyuo vyao ili kuweza kupata mafunzo ya darasani na kutembelea maeneo ambayo Japan wana vituo vya jotoardhi ili wapate ujuzi wa kufanya kazi na Wajapan na kutuletea ujuzi huo hapa nchini”, alisema Njombe.

Aidha, ameeleza kuwa kupitia ushirkiano huo na Serikali ya Awamu ya Tano Japan itaendelea kuisadia Tanzania katika kuendeleza nishati ya jotoardhi kwakuwa ni nishati yenye tija katika kutimiza ndoto za Tanzania kwa kuifanya kuwa nchi yenye kipato cha kati kufikia mwaka 2020.

Mhandisi Njombe aliongeza kuwa kwa niaba ya Serikali TGDC iko tayari kushirikiana na TOSHIBA ambapo Januari mwakani wataanza kuaninisha maeneo ya ushirikiano huo na kuyawekea muda wa utekelezaji na mwezi Machi Wataalam toka TGDC wataweza kwenda nchini Japan kwa ajili ya kwenda kupata elimu zaidi ya nishati hiyo.

Kwa upande wake Mtaalamu Mkuu toka Kampuni ya TOSHIBA Bwana Kentaro Kurahara ameeleza kuwa kampuni yao iko tayari kuisaidia Tanzania katika masuala yanayohusu jotoardhi na iko tayari kuomba ufadhili kupitia Serikali ya Japan ikiwemo kuwapa Wataalam wa TGDC elimu ya kutosha inayohusu nishati hiyo ili waweze kuhkikisha kuwa nishati hiyo inapatikana na kuleta maendeleo kwa Tanzania.

“Tunafuraha ya kushirikiana na TGDC katika kufanya tafiti zinazohusu jotoardhi kama mkataba wetu tuliousaini unavyosema, kupitia Serikali ya Japan na Shirika la JICA tutaomba ufadhili kwa ajili ya TGDC ili muweze kuleta wataalam wenu kuja kujifunza Japan pamoja kuwasaidia katika masuala mengine yanayohusu shughuli ya utafutaji wa nishati hii”, alisema Kurahara.

TGDC ni Shirika Tanzu lililopo chini ya Kampuni ya Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) ambapo limepewa lengo na Serikali la kuharakisha upatikanaji wa nishati ya jotoardhi kufikia Megawati 200 mwaka 2020.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 13053

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>