Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia maelfu ya wakazi wa Mwanza na miji ya jirani katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza jana jioni.Rais Kikwete yupo Mkoani Mwanza kwa ziara ya kikazi kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo. Picha na Freddy Maro
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumapili, Septemba 8, 2013, amezindua mtambo wa kufua umeme kiasi cha megawati 60 katika eneo la Nyakato mjini Mwanza, umeme ambao utachangia kwa kiwango kikubwa kupunguza shida ya umeme katika Mkoa wa Mwanza na mikoa ya jirani.
Aidha, Rais Kikwete ameiangiza Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuanza mara moja maandalizi ya kupeleka umeme kwenye machimbo ya madini ya nikeli yaliyoko Kabanga, Ngara, Mkoa wa Kagera.
Vile vile, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake itaharakisha mipango ya kujenga reli hadi kwenye eneo hilo kama maandalizi ya kuanza kuchimbwa kwa madini hayo ambayo ni mazito na kuyasafirisha kwa barabara kwenda bandarini Dar Es Salaam kutaharibu kwa haraka barabara zinazojengwa kwa gharama kubwa nchini.
Akizungumza kabla ya kuzindua mtambo huo, Rais Kikwete ameitaka Wizara ya Nishati na Madini kuharakisha mipango ya kuunganisha eneo la Kabanga, Ngara, Mkoani Kagera kwenye Gridi ya Taifa ili uzalishaji wa madini ya nikeli usije kukwamishwa na ukosefu wa umeme. Amesema kuwa mgodi huo utahitaji umeme mwingi kiasi cha megawati 40.
Rais amesema kuwa Serikali yake itahakikisha inafikisha reli kwenye eneo la Kabanga mapema ili kuhakikisha kuwa nikeli inayozalishwa inasafirishwa kwa reli badala ya barabara. Amesema kuwa madini hayo ni mazito mno na kuyasafirishwa kwa barabara kutaharibu kabisa na katika muda mfupi barabara ambazo zinajengwa nchini kwa gharama kubwa.

Akizungumza na wananchi kwenye sherehe ya uzinduzi huo, Rais Kikwete amesema kuwa umeme siyo anasa bali ni moja ya vigezo vya msingi na muhimu kabisa vya maendeleo.

“Nc hi yetu ya Tanzania ina umeme kiasi cha megwati 1,450 tu wakati katika Afrika Kusini ni megawati 45,000 na unaweza kuona tofauti ya maendeleo. Hivyo, ni muhimu sana kwetu kuongeza kiwango cha kuzalisha umeme katika nchi yetu.”
Katika siku ya tatu ya ziara yake kukagua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Mwanza, Rais Kiwete pia amefungua Kituo cha Polisi cha Nyakato ambacho kimegharimu sh milioni 450, Serikali ikiwa imechangia kiasi cha asilimia 20 cha gharama hizo.
Kituo hicho cha kisasa kilianza kujengwa mwaka 2003 lakini ujenzi wake ukawa unakwamakwama kutokana na ukosefu wa bajeti hadi uongozi wa polisi wa Mkoa wa Mwanza ulipoamua kukijenga kituo hicho kwa njia ya kuishirikisha jamii na ikaundwa Kamati ya Ujenzi chini ya uenyekiti wa Bwana Alfred Wambiura.
Akizungumza kwenye sherehe ya ufunguzi wa kituo hicho, Rais Kikwete ameahidi kuwa atajenga nyuma moja kwa ajili ya mkazi ya polisi. Kituo hicho kina jumla ya askari polisi 65.