Mshambuliaji wa Simba, Mwombeki Betram, akimtoka beki wa Mgambo Bakari Mtama, wakati wa mchezo wa ligi kuu ya Vodacom uliochezwa leo jioni kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam. Katika mchezo huo Simba imeibuka na ushindi mnono wa mabao 6-0.
Mabao ya Simba leo yametupiwa kambani na Amisi Tambwe, aliyetupia mabao 4 na Haruna Chanongo, mabao 2, ambayo yameiwezesha timu hiyo sasa kukalia usukani uliokuwa umeng'ang'aniwa na JKT Ruvu, ambao leo wamechezea kichapo cha bao 1-0 na Ruvu Shooting.
Wakati Simba wakifululiza kwa ushindi katika mechi zake mbili, watani wao Yanga nao wameendelea kufululiza kwa sare wakiwa huko ugenini Jijini Mbeya baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na timu ya Tanzania Prisons.
Huko Chamazi, wazee wa Lambalamba, Azam Fc, nao wamelazimishwa sare ya bao 1-1 na Wauza Mitumba wa Ilala, Ashanti United.
Nao Timu ya wakata Miwa wa Kagera Sugar, wakiwa katika Dimba la nyumbani Kaitaba mjini Bukoba, wameibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Wajeda wa Arusha JKT Oljoro.
Wakata Miwa wa Turiani Mtibwa Suger, nao wamelazimishwa sare ya 0-0 Watoto wa Mbeya City.
Wagosi wa Kaya Coastal Union ya Tanga, wakiwa dimba la nyumbani Mkwakwani, nao wamelazimishwa sare ya 1-1 na Wajeda wa Tabora Rhino Rangers.