PICHA KWA HISANI YA BIN ZUBEIRY BLOG
TIMU YA Zanzibar Heroes, leo imejiweka katika hati hati ya kwenda au kutokwenda Robo Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Chalenji baada ya kuchapwa mabao 3-1 na Ethiopia mchana wa leo, Uwanja wa Nyayo, Nairobi, Kenya.
Mabao yaliyoizamisha Zanzibar leo yalifungwa na nahodha, Fasika Asfan dakika ya tano, Salahadin Bargicho kwa penalti dakika ya 37 baada ya Manaye Fantu kuangushwa kwenye eneo la hatari wakati Yonathan Kebede alifunga la tatu dakika ya 83.
Bao la Zanzibar lilifungwa na kiungo mpya wa Simba SC, Awadh Juma Issa dakika ya 68 kwa kichwa akiunganisha krosi ya Seif Abdallah Karihe, ambaye alimlamba chenga beki wa kulia wa Ethiopia kwanza.
Zanzibar ilipata pigo mapema tu dakika ya 14, baada ya mchezaji wake tegemeo Suleiman Kassim ‘Selembe’ kuumia nyama za paja na kutoka nje, nafasi yake ikichukuliwa na Seif Abdallah Karihe.
Kwa kipigo cha leo, Zanzibar inabaki na pointi zake tatu ilizovuna kwa kuifunga Sudan Kusini 2-1 katika mchezo wa ufunguzi na Ethiopia iliyoanza kwa sare ya bila kufungana na wenyeji Kenya, inakuwa na pointi nne.