*****************************************************
Na Frank Mvungi
TAASISI yaTiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) imepanga kutumia zaidi ya Bilioni 17 katika ujenzi wa awamu ya Tatu ya Mradi wa Taasisi yaTiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI phase 111) hadi mradi huo utakapokamilika mapema mwakani.
Hayo yamesemwa leo na Meneja Uhusiano wa Taasisi hiyo Bw. Jumaa Almasi wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Almasi alisema kuwa Ujenzi wa jengo hilo jipya lenye ghorofa 7 ambao unaendelea ukikamilika utaongeza maeneo ya kutolea huduma,Vitanda vitafikia 380 kutoka 159 vilivyopo sasa hali ambayo itapanua wigo wa huduma zinazotolewa kwa sasa.
“Mradi huu utasaidia kuongeza ufanisi na huduma zinazotolewa na taasisi kwani ukikamilika utaongeza maeneo ya kutolea huduma kwa kupunguza msongamano wa wagonjwa mawodini kutokana na kuongezeka kwa vitanda kutoka 159 hadi kufikia 380” Alisema Almasi.
Aliongeza kuwa huduma nyingine zitakazotolewa ni CT SCAN,MRI,huduma za Cybernife na Digital Antiograph ambazo kwa Sasa hazitolewi katika Taasi hiyo .
Alibainisha kuwa MOI ni moja ya Taasisi zenye vifaa bora vya upasuaji pamoja na vyumba vya upasuaji vinavyokikidhi viwango vya kimataifa kusini mwa jangwa la Sahara baada ya Afrika ya kusini.
Alisema kuwa hali hiyo ni matokeo ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kuboresha huduma za afya nchini ambapo wameweza kupatiwa vifaa vya kisasa pamoja na wataalamu waliobobea katika huduma za tiba ya mishipa ya fahamu na upasuaji wa uti wa mgongo.
Bw. Almasi alibainisha kuwaTaasisi ya MOI imeendelea kushirikiana na Taasisi za Kimataifa zinazotoa huduma za afya kama SIGN GROUP ya nchini Marekani ambayo imekuwa ikitoa msaada wa vifaa tiba ikiwa ni alama ya ushirikano mzuri uliopo kati ya Taasisi hiyo na mashirika ya Kimataifa.