Na Mwandishi Wetu, Dar
WAKALI wa muziki wa dansi nchini Extra Bongo Next Level 'Wazee wa Kizigo' wamerejea jijini Dar es Salaam kwa kishindo baada ya kuhitimisha ziara ya wiki moja ya maonyesho katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa huku wakiacha gumzo baada ya kufanikiwa kukata kiu ya burudani kwa mashabiki wa muziki wa dansi.
Akizungumza na mtandao huu jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa bendi hiyo Kamarade Ally Choki, alisema, ziara yao ilikuwa ni ya mafanikio makubwa kwao baada ya idadi kubwa ya mashabiki kujitokeza kwenye maonyesho ya sikukuu za mwisho wa mwaka ambapo Extra Bongo ilitikisa Mikoa ya Geita, Kagera, Biharamulo Kahama na Mkoani Shinyanga.
Katika ziara hiyo iliyopewa jina la safari ya 'Mafahari watatu' wanamuziki Mwinjuma Muumini 'Kocha wa Dunia', Ramadhani Masanja 'Banza Stone' na Choki walifanikiwa kukumbusha enzi hizo walipounda umoja wao ulioitwa Mafahari Watatu na kutoa albamu iliyoitwa 'Golden Albam' kwa kuimba nyimbo kadhaa nyingi zikiwa za Extra Bongo.
Miongoni mwa nyimbo zilizopamba ziara hiyo ni 'Barua', 'Ufisadi wa Mapenzi', Mtenda Akitendewa', 'Double Double', 'Nguzo tano za Mapenzi', 'Mgeni', 'Hafidhi' na 'Regina Zanzibar' huku Muumini pia akiwanogesha kwa kuimba nyimbo kama 'Tunda', 'Kilio cha Yatima' na 'Utafiti wa Mapenzi' wakati Banza alipagawisha maonyesho hayo kwa kuimba Mega Mix ya nyimbo kama 'Angurumapo Simba', 'Mtaji wa masikini' na 'Elimu ya Mjinga'.
Choki alisema wamefarijika sana na ziara hiyo kwakua imeonyesha jinsi gani wanavyokubalika kwani wapenzi wengi licha ya kuguswa na sauti za waimbaji wake walionyeshwa kukunwa na shoo kali za safu ya unenguaji wao chini ya Super Nyamwela na Otilia Boniface.
Alisema wamerejea jijini Dar es Salaam ambapo Alhamisi wataanza kuwapa burudani mashabiki wao kwenye Ukumbi wa Chitaz uliopo Sayansi Kijitonyama, Ijumaa Urafiki na Jumamosi uwanja wa nyumbani Meeda huku akiwataka wapenzi na mashabiki wao kujitokeza kwa wingi kupata baadhi ya vionjo vipya walivyojifunza kutoka Mikoani.