WAKATI uchaguzi wa Mwenyekiti wa kudumu wa Bunge Maalumu la Katiba ukitarajiwa kufanyika leo jioni mjini Dodoma, tayari wagombea wawili waliojitokeza kuchukua fomu ya kutaka kuwania nafasi hiyo, wameenguliwa baada ya kushindwa kurudisha fomu ya kuwania nafasi hiyo kwa muda uliopangwa.
Wajumbe hao ni pamoja na Dkt. Theresya Huvisa pamoja na Danstan Chipaka wameenguliwa katika kinyang’anyiro hicho kufuatia kushindwa kurudisha fomu za kugombea ambazo zilipaswa kurudishwa leo saa 4 asubuhi.
Kufuatia kuenguliwa kwa wajumbe hao, nafasi hiyo sasa itawaniwa na Samwel Sitta pamoja na Hashim Rungwe, ambao ndiyo waliokidhi vigezo kwa kuchukua fomu na kurudisha kwa wakati.
Uchaguzi wa Mwenyekiti unatarajiwa kufanyika leo saa 10 jioni, ambapo baada ya kutangazwa matokeo kutatangazwa uchukuaji fomu kwa wajumbe watakaotaka kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, ambaye kulingana na kauli za mwenyekiti wa muda aliyepita kuzingatia 'Jenda' atakuwa ni mwanamke.
Mpaka sasa anayetajwa kutarajiwa kuwania nafasi hiyo ya Makamu Mwenyekiti, ni Samia Suruhu.
Kwa mujibu wa kanuni za Bunge Maalumu la Katiba, Makamu Mwenyekiti wa Bunge anapaswa kutoka upande wapili wa muungano iwapo Mwenyekiti atakuwa amechaguliwa kutoka upande mwingine wa muungano ili kuleta usawa.