Na Mwandishi Wetu, Mtwara
MKUU wa Wilaya ya Mtwara Mjini, Mh. Wilman Ndile amewataka wananchi wa wilaya yake na mkoani Mtwara kwa ujumla, kujitokeza kushiriki semina ya ujasiriamali itakayofanyika mwishoni mwa wiki hii wilayani kwake ili kujikomboa kiuchumi.
Ndile alisema, hiyo ni fursa ya kipekee kwa wananchi wa Mtwara kujitokeza kushiriki semina hiyo itakayofanyika kesho kutwa Ijumaa (tarehe 26 Julai) hadi Jumatatu ya 29 Julai mwaka huu kwenye Ukumbi wa Chuo cha Ualimu Mtwara (TTC) ili waweze kuboresha maisha yao.
Akizungumza jana mkoani hapa, Ndile alisema kupitia mafunzo hayo, wananchi wa Mtwara watakuwa katika nafasi nzuri ya kuweza kujenga uchumi wa nchi na kutoka katika hali ya utegemezi.
“Watu wengi hawana njia nyingine ya kujiingizia kipato, sasa kwa kushiriki mafunzo haya wataweza kupata ujuzi utakaowawezesha kuzalisha bidhaa ambazo wataziuza na kujiongezea kipato,” alisema Ndile.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Mod Integrated Solutions an Awareness, Mahmoud Komba, ambao ndiyo waandaaji wa semina hiyo, alisema mafunzo yatawawezesha washiriki kutengeneza bidhaa mbalimbali za viwandani na kilimo kama sabuni za aina zote, mafuta ya kujipaka, lotion za aina zate, mishumaa ya aina zote, poda (Powder) zitokanazo na mihogo na masomo mengine ya kilimo.
Alisema katika semina hiyo iliyodhaminiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) washiriki watatakiwa kuchangia gharama kidogo ili waweze kushiriki na kujipatia vyeti.
“Wananchi wanatakiwa kujitokeza kwa wingi siku ya Ijumaa wiki hii huku wakichangia kiasi kidogo cha fedha ili waweze kupata elimu ya utengenezaji wa bidhaa hizi za kilimo na kiwandani ili waweze kujikwamua kiuchumi,” alisema Komba.