Wachezaji wa timu ya taifa 'Taifa Stars' na Uganda 'The Cranes', wakiingia uwanjani tayari kwa kuanza mechi yao ya marudiani ya kufuzu kucheza fainali za Chan mwakani zitakazofanyika nchini Afrika ya Kusini. Mchezo huo umechezwa leo kwenye uwanja wa Mandela, Namboole mjini Kampala, Uganda. Katika mchezo huo, Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, imefungwa mabao 3-1.
Kwa matokeo hayo sasa Stars, imeondolewa katika mbio hizo za kuwania kufuzu kucheza fainali za Chan, huku Uganda 'The Cranes' ikifuzu na kutinga katika fainali hizo baada ya kuibuka na jumla ya mabao 4-1 baada ya mchezo wa kwanza uliopigwa Jijini Dar, na timu hiyo iliibuka na ushindi wa bao 1-0. Bao la kwanza la Uganda lilifungwa na Frank Kalanda, katika dakika ya 7 na Dakika ya 18, Amri Kiemba, aliisawazishia Stars.
Uganda ilipata bao la pili katika dakika ya 48 kupitia kwa Brian Mjegwa, kwa njia ya mkwaju wa penati baada ya mchezi wa stars kuunawa mpira katika eneo la hatari na bao la tatu lilifungwa katika dakika ya 63 baada ya Kiungo wa Stars, Salum Abubakar, 'Sure Boy' kupokonywa mpira na adui.
Katika dakika ya 32, Mrisho Ngassa, aliachia shuti kali lililomshinda kipa wa Uganda na kugonga mwamba wa juu na kutoka nje.
Kocha wa Taifa, Kim Poulsen, alifanya mabadiliko, kwa kumtoa Frank Domayo aliyeumia na kumuingiza Simon Msuva. Mabadiliko mengine, alitoka Beki wa kushoto, David Luhende na nafasi yake ikachukuliwa na Vicent Barnabas na John Boko nafasi yake ikachukuliwa na Haruna Chanongo, mabadiliko ambayo hayakuweza kuzaa matunda.
Kikosi cha kwanza cha timu ya Taifa, 'Taifa Stars', Kikosi kilikuwa ni Juma Kaseja, Erasto Nyoni, David Luhende, Kelvin Yondani, Agrey Morris, Athumani Idd ''Chuji', Mrisho Ngassa, Frank Domayo, Salum Abubakar, Amri Kiemba na John Boko.
Kikosi cha timu ya Uganda 'The Cranes'.
Kiungo mshambuliaji wa Taifa Stars, Amri Kiemba, akiwatoka mabeki wa Uganda huku akizongwa na beki wa Uganda Cranes, Nicolas Kadada.
Mchezaji wa Taifa Stars Aggrey Morris (katikati) akiwania mpira na mabeki wa Uganda Cranes.
Sehemu ya mashabiki wa Taifa Stars wakishangilia goli la kusawazisha.
Amri Kiemba akipongezwa na Mrisho Ngasa/ Aboubakar Salum 'Sure Boy' baada ya kushinda bao la kusawazisha dhidi ya Uganda Cranes.
Mrisho Ngassa akiwania mpira na beki wa Uganda Cranes, Sabit Kabugo.
David Luhende akiambaa na mpira huku beki wa Uganda Cranes Said Kyeyune akijaiandaa kumkabili.
Mrisho Ngasa akiwania mpira na Nicolas Kadada wa Uganda Cranes.
*********************************
Na Boniface Wambura, Uganda
Tanzania (Taifa Stars) imeshindwa kufuzu Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) kwa mara ya pili mfululizo baada ya leo (Julai 27 mwaka huu) kufungwa mabao 3-1 na Uganda Cranes, hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 4-1.
Stars ambayo ilicheza fainali za kwanza zilizofanyika Ivory Coast mwaka 2009 ilimaliza kipindi cha kwanza katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa wa Mandela ulioko Namboole nje kidogo ya Kampala ikiwa sare ya bao 1-1.
Wenyeji ndiyo walioanza kufunga bao dakika ya saba katika mechi hiyo iliyochezeshwa na Kanoso Abdoul Ohabee kutoka Madagascar. Frank Kalanda alifunga bao hilo akimalizia mpira uliopigwa ndani ya eneo la hatari la Tanzania.
Bao hilo halikuonekana kuichangaza Taifa Stars, kwani ilitulia na kufanikiwa kusawazisha dakika ya 18 mfungaji akiwa Amri Kiemba kutokana na pasi nzuri ya Mrisho Ngasa kwenye kona ya eneo la mita 18.
Dakika ya 32 nusura Taifa Stars ipate bao, lakini mkwaju maridadi wa Mrisho Ngasa ambao tayari ulikuwa umempira kipa HAmza Muwonge uligonga mwamba kabla ya kuokolewa na mabeki wa Uganda Cranes.
Mabao mengine ya Uganda Cranes yalifungwa dakika ya 48 kupitia kwa Brian Majwega na lingine dakika ya 63 mfungaji akiwa tenda Kalanda kutokana na makosa ya Salum Abubakar kupokonywa mpira wakati akiwa katika nafasi nzuri ya kutoa pasi kwa mwenzake.
Kocha Kim Poulsen alifanya mabadiliko dakika ya 43 kwa kumuingiza Simon Msuva badala ya Frank Domayo aliyeumia, na dakika ya 78 akawaingiza kwa mpigo Haruni Chanongo na Vincent Barnabas badala ya David Luhende na John Bocco. Hata hivyo mabadiliko hayo hayakubadili matokeo ya mchezo.
Kikosi cha Stars kilipangwa hivi; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, David Luhende/Vincent Barnabas, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Athuman Idd, Frank Domayo/Simon Msuva, Salum Abubakar, John Bocco/Haruni Chanongo, Amri Kiemba na Mrisho Ngasa.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itarejea nyumbani kesho (Julai 28 mwaka huu) saa 4 usiku kwa ndege ya PrecisionAir.