Na Magreth Kinabo – Maelezo
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospete Muhongo amesema kwamba kuanzia sasa hakuna mgodi utakaoanzishwa bila ya serikali kuwa na hisa .
Kauli hiyo imetolewa leo na Profesa Muhongo wakati wa utiaji saini leo makubaliano ya kukabidhi mgodi wadhahabu wa Tulawaka kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kutoka kwa Kampuni ya Uchimbaji wa Madini ya Afrikan Barrick Gold (ABG) katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa wizara hiyo jijini Dares Salaam.
Utiaji saini huo ulifanywa na Mkurugenzi Mkuu wa STAMICO,Gray Mwakalukwa na Makamu wa Rais wa ABG, Deo Mwanyika.
“STAMICO itachimba katika mgodi huo kwa niaba ya Watanzania, hivyo serikali itaiwezesha kiutendaji, kifedha,kiutalaamu na kuwa na rasimali watu, alisema Profesa Muhongo.
Aliongeza kuwa baadae shirika hilo litauza hisa kwa Watanzania.
Alisema STAMICO imenunua mgodi huo kwa dola za Marekani milioni 4.5, ambapo kati ya fedha dola milioni 3.5 zimeshalipwa moja kwa moja.
Akizungumzia kuhusu uuzaji wa mgodi huo, Mwanyika alisema kulingana na sera zao uchimbaji huo hautakuwa na faida kwao , hivyo eneo hilo linafaa kuendelezwa na wachimbaji wa kati.
Alisema STAMICO itachukua mdogi huo na baaadhi ya leseni za utafutaji wa madini zinazozunguka eneo hilo kwa gharama hiyo na kukubali kutoa asilimia 2 ya mrabaha iwapo uzalishaji utazidi wakia 500,000 zikiwa na kikomo cha dola za Marekani 500,000.
Mwanyika alifafanua kwamba STAMICO itachukua umiliki na usimamizi wa mfuko wa fedha za ukarabati wa mazingira ikiwa kama sehemu ya mpango wa ufungaji wa mgodi huo na itakuwa na dhamana ya majukumu yaliyopita na ya baadae yanayohusiana na kufunga mgodi na ukarabati wa mazingira.
Aidha itawajibika kulipa fidia kwa wahusika wengine wa mkataba huo iwapo majukumu yao yalioainishwa hayakutekelezwa na ABG itailipa STAMICO salio lililobakia kwenye mfuko wa kukarabati mazingira ambayo kwa sasa ni dola za Marekani milioni 17.6,ambapo bei pia ya mauzo kwenye makubaliano itapunguzwa kutoka kwenye salio.
Katika hatua nyingine Profesa Muhongo alisema watu wenye maeneo makubwa ya vitalu vya madini ambayo hawajayafanyia kazi yatachukuliwa kulingana na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na watapewa wachimbaji wadogo.
Alisema STAMICO itakuwa inawasimamia wachimbaji wadogo, itawasaidia kupata mikopo kiurahisi kutoka Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), kutoa elimu ya uchimbaji na kuhifadhi mazingira kupitia vyama vyao.